MASHITAKA 11 dhidi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe,
yamebainisha kuwa kosa kubwa la kiongozi huyo kijana, ni nia yake ya
kutaka kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.
Chanzo
chetu cha habari kilichoona mashitaka hayo kabla ya kutumwa kwa
washitakiwa, kimebainisha kuwa makosa saba kati ya makosa 11, yanahusu
kugombea uenyekiti Taifa, au kumkashifu Mwenyekiti wa Taifa.
“Ukiona
hayo mashitaka yenyewe ndugu yangu, yanajirudia rudia na kuzunguka
katika kosa moja la nia ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa…
angalia kosa la kwanza, kosa la tatu, tano, sita nane na tisa, ni kama
vile kuwania uenyekiti ndio kosa kubwa.
“Hata
hivyo kwa jinsi mgawanyiko ulivyo ndani ya chama sasa, nakuhakikishia
hawa jamaa (Zitto, Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba), watarudishwa
katika nyadhifa zao na hakuna atakayeadhibiwa,” alisema mtoa taarifa
wetu.
Alinukuu
kauli ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu
aliyehoji kama makosa wanayotuhumiwa akina Zitto ni makubwa kiasi cha
kuyeyusha mema aliyoyafanya katika chama. “Si umesikia akina Baregu
wakizungumza? Kwa mashitaka yale nakuhakikishia kitakachofanyika ni
kufunika kombe mwanaharamu apite,” alisema mtoa habari wetu.
Kosa
la kwanza kwa Zitto, Dk Mkumbo na Mwigamba, wanadaiwa kuvunja Kanuni ya
Chama inayokataza kukashifu chama, kiongozi au mwanachama yeyote.
Katika maelezo ya kosa hilo, akina Zitto wanadaiwa kumkashifu Mwenyekiti
wa Taifa, Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Mjumbe wa Kamati
Kuu, Godbless Lema.
Moja
ya madai katika mashitaka hayo, ni kilichoandikwa katika Mkakati wa
Mabadiliko 2013, kuwa Mbowe amekuwa akinunua vifaa vyote vya chama nje
ya nchi kwa bei anayoijua mwenyewe na ambayo haihojiwi popote. Wanadaiwa
pia wamemkashifu Dk Slaa kwa kudai ni mdhaifu kwa kumruhusu Mbowe
kuingilia shughuli za kiutendaji.
Zitto
na wenzake wanadaiwa katika kosa la pili, kutokuwa wawazi na wa kweli
wakati wote na kushirikiana na vikundi vya majungu na udanganyifu
kinyume na Kanuni za Uendeshaji kipengele cha 10.1 (VIII. Katika kosa la
tatu, wanadaiwa kutoa tuhuma juu ya viongozi wenzao bila kupitia vikao
halali na utaratibu wa ngazi zilizowekwa, kinyume na kanuni ya 10.1 (X).
Katika
kosa la nne, akina Zitto wanadaiwa kujihusisha na vikundi vyenye
misingi ya ukabila, udini au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana
ndani ya chama, miongoni mwa jamii, kisiasa au kijamii. Katika kosa hilo
wanadaiwa kwenda kinyume na kipengele cha 10.1 (IV), cha Kanuni za
Uendeshaji wa Chama.
Akina
Zitto katika kosa la tano, wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya
kuchonganisha na kuzua migogoro kwa viongozi wa chama au wanachama,
kinyume na kifungu cha 10.1 (IX), cha Kanuni za Uendeshaji wa Chama.
Katika
kosa la sita ambayo mtoa habari wetu alisema ndio kubwa, Zitto na
wenzake wanadaiwa kutekeleza mpango wa kusudio la kugombea uenyekiti wa
Chama Taifa, bila kutangaza kusudio la kutangaza nafasi hiyo.
Hatua
hiyo inadaiwa kuwa ni kinyume na kifungu 2.C cha Muongozo wa Kutangaza
Kusudio la Kuwania Nafasi ya Uongozi wa Chama, Mabaraza na Serikali wa
2012.
Zitto
na wenzake katika kosa la saba, wanadaiwa kutengeneza mitandao ya
kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya kujihakikishia ushindi kinyume
na kanuni ya 2 (D), ya Muongozo wa Kuwania Uongozi. Katika kosa la
nane, Zitto na wenzake wanadaiwa kuwachafua viongozi na wanachama
wengine wenye kusudio/nia ya kutaka kugombea nafasi ya uenyekiti kinyume
na kifungu 2 (E) cha Muongozo wa Kuwania Uongozi.
Katika
kosa hilo, kumewekwa maelezo ya ziada kuwa kosa hilo linaunganishwa na
kosa la kwanza ambalo washitakiwa wanadiwa kuwakashifu Mbowe, Dk Slaa na
Lema.
Kosa
la tisa, akina Zitto wanadaiwa kujihusisha na upinzani dhidi ya chama
na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa
uchaguzi wa chama, kinyume na kifungu cha 10.3 (IV), cha Kanuni za
Uendeshaji.
Kosa
la kumi linamhusu Zitto peke yake, ambapo anaidaiwa kukashifu chama na
kiongozi wa chama nje ya Bunge kinyume na kifungu 2 C (B), kikisomwa
pamoja na kifungu 3 B cha Kanuni za Mwenendo wa Maadili ya Wabunge.
Katika
hilo Zitto kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa chama yaani Dk
Mkumbo na Mwigamba na mtu mwingine ambaye hajajulikana, wanadaiwa
kusambaza waraka uitwao Mkakati wa Mabadiliko 2013.
Mkakati
huo, unadaiwa kukashifu chama na/ au viongozi wake wakuu kama
ilivyoelezwa katika kosa la kwanza, tatu, nne na nane. Mwisho katika
kosa la 11, Zitto na wenzake wanadaiwa kuchochea mgawanyiko ndani ya
chama kinyume na kanuni ya 3 F ya Kanuni za Mwenendo wa Maadili ya
Bunge.
Katika
hali inayoonesha muendelezo wa kupukutika kwa chama hicho, jana mkoani
Mwanza kulianzishwa kinachoitwa Muunganiko wa Wawakilishi wa Matawi 189
ya Chadema katika mkoa huo.
Taarifa
ya kiongozi wa Muungano huo, Robert Gwanchele, kwa vyombo vya habari,
ilibainisha kuwa unawajumuisha wajumbe kutoka majimbo yote ya mkoa wa
Mwanza na lengo ni kupinga hatua za Kamati Kuu dhidi ya Zitto na
wenzake.
Kuibuka
kwa muungano huo katika mkoa muhimu kisiasa kwa Chadema, kunaonesha
kuwa chama hicho kinaelekea kupata pigo kwa wanachama kuanza kugawana
makundi mawili yaliyoibuka katika chama hicho yanayoongozwa na wagombea
uenyekiti; kundi la Mbowe na Zitto.
“Katika
kikao chetu tulichoketi Novemba 30, 2013 kuanzia saa nne asubuhi mpaka
saa tisa kasorobo, pamoja na mambo mengine tumeazimia kuanzisha umoja
huu wa wanachama.
“Hii
ni kutokana na ukweli kwamba viongozi wetu wanaotuwakilisha kwenye
vikao vya uamuzi kama vile wilaya, mkoa na taifa, wamekuwa waoga na
wameshindwa kuwakilisha mawazo yetu tuliyowatuma badala yake wengi wao
wamekubali kuwa vibaraka wa kile kinachoitwa Chadema Kaskazini,”
ilieleza taarifa ya kundi hilo linalomuunga mkono Zitto.
Kundi
hilo dhidi ya upande wa Mbowe Mwanza, limeeleza kuwa sababu
zilizotolewa na Kamati Kuu kwa ajili ya kumuadhibu Zitto na wenzake,
hazikubaliki na kutoa walizoziona kuwa ndio sababu za kuandamwa kwa
kiongozi wao.
Kwa
nini Zitto? “Uamuzi wa Kamati Kuu wa Novemba 20-21 mwaka huu wa kuwavua
uongozi Zitto Kabwe, Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, umeonesha
dhahiri si woga tu wa demokrasia, bali ni unafiki wa hali ya juu kwa
viongozi wetu kukwepa demokrasia kwa kisingizio cha usaliti na uhaini
ndani ya chama,” taarifa hiyo ilieleza. Taarifa hiyo iliyotolewa na
Gwanchele, ilieleza sababu za kuandamwa kwa akina Zitto kuwa ni kutaka
kujua mapato na matumizi ya fedha za chama zinazotokana na ruzuku ya
fedha za serikali.
Nyingine
ni michango ya wanachama na wapenzi kwenye mikutano ya wazi, harambee
za Operesheni ya M4C Mwanza, Arusha na Dar es Saalam na kutaka kujua
taratibu za ununuzi wa rasilimali za chama na namna wazabuni wa
kusambaza bendera, kadi za chama, magari na pikipiki walivyopatikana.
Nyingine ni kutaka kuona usawa wa kimadaraka kwa viongozi wote bila
ubaguzi wa aina yoyote, kuanzia ngazi ya chini mpaka Taifa kinyume na
ilivyo sasa hasa makao makuu ya chama ambapo ilidaiwa ukanda na ubaguzi
wa hali ya juu umetawala.
“Mwenyekiti
na Katibu Mkuu, wameshindwa kutatua migogoro ya viongozi na wanachama
kutoka mikoani kwa njia sahihi za vikao na kwa wakati, hivyo kutoa
mwanya kwa viongozi na wanachama kutumia njia ya mitandao ya kijamii
tukiongozwa na Katibu Mkuu mwenyewe, kujitokeza mara kwa mara kwenye
mitandao hiyo hiyo kwa madai ya kutolea ufafanuzi wa mambo mbalimbali
yahusuyo masuala ya chama, ilihali akijua kufanya hivyo ni usaliti
mkubwa kwa chama chake,” ilidai taarifa hiyo.
Gwanchele
alidai katika taarifa hiyo kuwa njia hiyo ya Dk Slaa kutoa ufafanuzi wa
mambo ya chama katika mitandao, ndiyo iliyosababisha migogoro mikubwa
hususan katika mkoa wa Mwanza, iliyochangia kupoteza Halmashauri ya Jiji
la Mwanza, baada ya kufukuzwa kwa baadhi ya madiwani.
“Tunataka
kujua hatua gani zilizochukuliwa dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema, kumkashifu kiongozi wa chama Zitto Kabwe kuwa ni mnafiki
na mzandiki kwenye mitandao ya kijamii,” ilieleza taarifa hiyo ya
Gwanchele ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Matawi ya Chadema Mkoa wa
Mwanza, Mwenyekiti wa Vijana Kanda ya Chama Ziwa Magharibi na Mjumbe
Kamati Tendaji Wilaya Ilemela.
“Tunataka
kujua hatua gani zilizochukuliwa na chama dhidi ya Henry Kilewo
(Mkurugenzi Chadema) kwa kuweka waraka unaoitwa ripoti ya siri
inayomhusu Zitto ambao chama makao makuu kupitia kwa Mkurugenzi wa
Habari na Uenezi kimeukana mbele ya vyombo vya habari,” ilieleza taarifa
hiyo.
Kilewo,
ambaye pia ni kiongozi wa chama ngazi ya mkoa wa Kinondoni kichama,
anadaiwa aliweka waraka huo kwenye Blog yake wakati akijua kufanya hivyo
ni kinyume na kanuni za viongozi wa chama kuhusu maadili ya viongozi
kanuni ya 10.
“Tunataka
kuona nguvu iliyotumika kuwaadhibu Zitto na wenzake kwa kuandaa waraka
ujulikanao kama mkakati wa mabadiliko 2013, nguvu hiyo hiyo itumike kwa
hawa waliotumia njia chafu ya kuandaa waraka wa kumchafua Zitto ambao
chama kinawajua na baadhi yao tumewaweka humu kwenye tamko letu.
“Kingine
tunataka kwa mara nyingine viongozi wa chama makao makuu wauambie umma
wa Watanzania ni kwanini waraka huo huo unaoitwa waraka wa siri kuhusu
Zitto, leo unagawiwa kwa viongozi na wanachama mikoani kwa agizo la
makao makuu… kama si ubaguzi ni nini?” Taarifa hiyo ilidai.
Katika
hitimisho lao, wanaumoja hao wametaka Mwenyekiti na Katibu Mkuu
wajiuzulu mara moja, ili kupisha uchunguzi wa mapato na matumizi ya
fedha za chama ambazo zinatokana na kodi za wavuja jasho. Pia
wamependekeza uamuzi wa Kamati Kuu ubatilishwe na mchakato wa kuwavua
uongozi akina Zitto ufuate taratibu na kanuni kwa mujibu wa Katiba.
Katika
utaratibu ule ule wa kauli za wafuasi wa Zitto kujibiwa na wafuasi wa
Mbowe, Katibu wa Vijana wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Florian Rwela,
alikanusha madai hayo. Rwela alisema Gwanchele kwa sasa ni mwanachama wa
kawaida anayetoka Kata ya Nyamanoro na kwamba zamani aliwahi kuwa
kiongozi lakini alivuliwa madaraka kwa mujibu wa taratibu za chama.
Alisema
hata kikao hicho cha wawakilishi wa matawi 189 si cha kweli kwa kuwa
hakiwezi kufanyika bila yeye kupata taarifa na mwenye mamlaka ya
kuratibu kikao cha namna hiyo, lazima atoke makao makuu.
Aliongeza
kuwa Gwanchele anaweza kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kama mwanachama,
lakini si kwa utaratibu wa kuratibu kikao cha namna hiyo.
Post a Comment