ASKARI Polisi wawili ambao picha yao
ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii wiki hii katika mkao wa uhusiano
wa kimapenzi, wamefukuzwa kazi. Picha hiyo ilionesha askari hao wa
Kikosi cha Usalama Barabarani wakiwa kwenye sare za jeshi hilo huku
mwanamume akiwa amempakata wa kike wakipigana busu.
Aidha askari mwenzao anayedaiwa kupiga
picha hiyo mwaka 2012 na kuisambaza kwenye mtandao wa kijamii, naye
amefukuzwa kazi. Polisi mkoani Kagera imesema imewafukuza kazi askari
hao watatu kwa kosa la kukosa maadili mema ya jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
mjini hapa, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Herny Mwaibambe alitaja
askari walio kwenye picha hiyo ni Namba F.7788 PC Mpaji Mwamsumbi na WP
8898 PC Veronica Mdeme, wote wa Wilaya ya Missenyi.
Aliyewapiga picha ni askari mwenye namba
G.2122 PC Fadhili Linga. Kwa mujibu wa Kamanda, walipiga picha mwaka
2012 wakiwa kazini kabla ya kusambazwa kwenye mitandao mbalimbali hivi
karibuni ikionesha Veronica akiwa amemkalia Mpaji mapajani. Kamanda
alisema picha hiyo inakwenda kinyume na maadili mema ya jeshi hilo.
Aidha alisema walipiga picha hiyo wakiwa
kazini na wamevaa sare za kazi. Kwa upande wa Fadhili, Kamanda alisema
anakabiliwa na kosa la kuwapiga picha wenzake hao kwa kutumia simu yake
ya kiganjani na kutuma kwenye mitandao mbalimbali wakati akijua ni
kinyume cha maadili ya Jeshi la Polisi.
Kosa lingine ni kutuma picha hiyo kwenye
mtandao. Alisema picha hiyo iliyoonekana kwenye mtandao ni picha halisi
ambayo haijachakachuliwa.
Alisisitiza kwamba maadili ya kijeshi
yapo kisheria na askari wao wanatambua. Alisema wanapokwenda vyuoni
wanafundishwa namna ya kuishi katika maisha ya utumishi wa Jeshi la
Polisi